Wednesday, April 16, 2014

DAKIKA 10 ZA PROFESA LIPUMBA ZILIZOWAONDOA BUNGENI WAJUMBE WA BUNGE MAALUM LA KATIBA JANA!


Mfululizo wa aya 13 za Mambo muhimu aliyoyazungumza njumbe wa bunge maalum la katiba Profesa Ibrahim Haruna Lipumba akichangia mjadala wa jumla wa sura ya 1 na ya 6 ya rasimu ya katiba jana dakika 11 kabla za kuwaongoza wajumbe wa bunge hilo wa kutoka upande wa upinzani maarufu kama UKAWA kutoka nje ya bunge kwa HASIRA.

“Mimi ni muumini wa dini ya mwenyezi Mungu, lakini naafiki mapendekezo yaliyoletwa kwetu na tume ya jaji Warioba ambayo ni tume iliyoundwa na rais”.

Gazeti la Mwananchi la tarehe 14/Aprili/2014, limeandika kuwa.. nanukuu “Waziri wa nchi ofisi ya Waziri mkuu sera, uratibu na bungeni mh. William Lukuvi ameanza kampeni kanisani, kuwataka wananchi kupinga serikali tatu zilizopendekezwa na tume ya mabadiliko ya katiba vinginevyo nchi itatawaliwa na jeshi kwa kuwa serikali ya muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi”. Hii ni kauli ya waziri Lukuvi ndani ya kanisa la Methodist wakati wa sherehe ya kumsimika mchungaji Joseph Bundala kuwa Askofu na waziri Lukuvi alikuwa anamuwakilisha waziri mkuu.”

“Zitto Kabwe asubuhi ya leo, ameeleza vizuri kwamba tatizo letu ni usmamizi mzuri wa mapato yetu ya nchi kwamba muungano kuvunjika hauvunjiki kwa sababu ya serikali 1, 2 au 3, ni utashi wa kisiasa na haya ni maneno pia, vice chancellor wangu Pius Msekwa alishayazungumza.”

“Kama ndugu zetu waz’bar, wangekuwa wanahitaji
muungano wa serikali moja, tungekuwa, na utaratibu mzuri tu wa serikali moja. Lakini siyo wanachama wa CUF,siyo wanachama wa CCM, waz’bar hawataki muungano wa serikali moja. Tume ya jaji Warioba kutoa mapendekezo ya serikali 3 ni kutokana na ukweli huo, hoja zinazoletwa hapa ni hoja za serikali 1 siyo hoja za serikali 2, lakini wenzetu serikali 1 hawataki. Kwa hiyo tunahitaji kuwa na muungano amabo tutakuwa na maridhiano ya pande zote mbili”.

“Wengi wamenukuu makala niliyoitoa katika kikao cha TCD, TCD iliunda baraza la katiba, na mimi nilichambua mapendekezo ya tume, nikasema kwa mapendekezo yaliyomo ndani ya rasimu ya katiba hayatakidhi mapato ya serikali ya shirikisho. LAKINI WANAONINUKUU WANAISHIA HAPO HAWAENDI KWENYE MAPENDEKEZO NILIYOTOA. Wamenisifu saana ni mchumi mahiri basi waendeleze sifa hizo kwa mapendekezo niliyoyatoa ya KUKIDHI MAHITAJI YA MAPATO YA SERIKALI YA SHIRIKISHO. Na nimeeleza, kwamba katika hali halisi, UTARATIBU MZURI NI MAPATO YA KILA SERIKALI KUCHANGIA MAPATO YA SHIRIKISHO na mambo haya yaandikwe ndani ya katiba. Katiba inaweza ikasema wazi 20% ya mapato yote yanayokusanywa Z’bar na yanayokusanywa Tanzania au Tanganyika yataenda kwenye serikali ya shirikisho. Na tuweke misingi mizuri ya kukusanya kodi na ya kutumia fedha za wananchi ndani ya katiba ya muungano ambayo ndiyo katiba mama. Na mambo haya yanawezekana.”

“Lakini ndugu zangu mjadala wetu unavyokwenda, utadhani rasimu iliyoletwa  na serikali, imeletwa ama na CUF au na CHADEMA au NCCR au Wapemba!”

“Ukurasa wa kwanza wa rasimu unaeleza kwamba  toleo hili la rasimu ya katiba linachapishwa kwenye gazeti la serikali kwa mujibu wa kifungu cha 20 (2) ya sharia ya mabadiliko ya katiba sura ya 83 na itawasilishwa kwenye bunge maalum la katiba kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na Jakaya Mrisho Kikwete rais. HII NI RASIMU YA TUME YA RAIS, siyo rasimu ya wapemba”.

“Lakini katika mjadala wetu hapa, Mjadala umekuwa na utaratibu wa ubaguzi!, watu wamebaguliwa humu, na VIONGOZI WAKUBWA WANAPIGA MAKOFI! Bunge hili limekuwa kama bunge la INTARAHAMWE! Hii ni HATARI kwa nchi yetu! Wapemba., Waarabu.., Wahindi.., Wakongo.., Wahadimu hii hatuhitaji ubaguzi katika nchi hii”.

“Tunahitaji katiba ambayo itahakikisha kila mwananchi anapata haki yake, wote tuwe sawa bila kujali rangi zetu, jinsia zetu, makabila yetu huu ndiyo msingi aliotuachia mwalimu Nyerere, tuuenzi msingi huo. Tusiweze kunza kufanya ubaguzi na ubaguzi umefanyaka ndani ya bunge hili”.

“Na kauli za waziri zinatisha zaidi, anapoeleza ndani ya kanisa kwamba waz’azr wanaotaka kuwa nan chi yao hawawezi kujitegemea, bali wanataka serikali ili wapate nafasi ya kujitangazia kuwa ni nchi ya Kiislamu. Waziri anaenda kusema hivyo ndani ya kanisa! Kawahamasisha mpaka yule kiongozi wa kanisa akaeleza kwamba, Askofu Bundala alisema kanisani hapo kwamba ili kudumisha muungano ni vyema katiba ya Z’bar ifutwe ili iwepo moja ya nchi moja ambayo inadumisha muungano, Mwisho wa kunukuu. Waziri wa nchi! na anakwenda kule kumwakilisha waziri mkuu, anatamka maneno kama haya!”.

“Sasa kama mlikuwa mnajua kwamba rasimu ya katiba ikipitishwa patakuwa na mapinduzi katika nchi, nchi haitatawalika, watu hawataweza kwenda kusali makanisani KWA NINI MLITULETA HAPA?, kwa nini mmetumia  BILLION 60, BILLION 70, Kwenye tume ya Jaji Warioba?, Kwa nini mmetufikisha hapa?

“Jengo hili naambiwa limekarabatiwa kwa shilingi BILLION 8.2, hali hamuiamini rasimu ya katiba! Ama ilikuwa utaratibu wa kupata hizo ‘Ten Percent’ ndiyo maana mmeratibu mmekarabati kwa gharama kubwa? Tunawataka.. CAG akague! Akague matumizi ya fedha zilizofanyika, Utatumiaje fedha nyingi wakati hiyo katiba inayowakilishwa kumbe hauitaki kabisa?”

“Tumechoka kusikiliza matusi! TUMECHOKA kudharau mawazo ya wananchi, TUMECHOKA ubaguzi. Hatuwezi kuwa sehaemu ya kundi la INTARAHAMWE linalohamaiisha ubaguzi ndani ya Tanzania, hili hatulikubali, hatulikubali, hatulikubali, watu wote tunaotaka katiba ya wananchi tunawaachia muendelee na kikao chenu.Ahsanteni sana".


Mara baada ya kusema hivyo, wajumbe waliounga mkono kauli yake waliinuka na kutoka nje.
Hata hivyo, kikao cha bunge hilo kiliendelea baada ya makamu mwenyekiti wa bunge hilo kusema idadi ya wajumbe waliobaki walitosha kuendelea na kikao hicho.

Wanaounga mkono muundo wa serikali tatu, wanasema muundo wa sasa wa serikali mbili umeshindwa kutatua masuala yenye mgogoro katika muungano, maarufu kama kero za muungano, hivyo kudhoofisha muungano huo.
Hata hivyo wajumbe wanaounga mkono serikali mbili, yaani serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanasema muundo wa serikali tatu ni kuvunja muungano wa Tanganyika na Zanzibar na pia itakuwa gharama kuiendesha serikali ya tatu.

Bunge hilo lenye zaidi ya wajumbe 600 linaundwa na wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la wawakilishi Zanzibar na wajumbe 201 walioteuliwa na rais wa Tanzania kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.

Wajumbe 191 kutoka upinzani walitoka nje ya bunge kupinga mwenendo wa bunge hilo katika kujadili rasimu ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
UNAWEZA SIKILIZA MCHANGO WA PROFESA IBRAHIM LIPUMBA HAPA CHINI