Kampuni ya Ufuaji Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imeanza utekelezaji wa mpango wake wa kuwezesha miradi mbalimbali kwa vijana wa Kitanzania kuimarika kiuchumi ikiwa na lengo la kukuza maendeleo ya uchumi nchini.
Akizungumza baada ya kukabidhi hundi ya Sh11 milioni kwa Kikundi cha Kwaya cha Kanisa la Mtakatifu Rita Wakashia lililopo Kimara, Dar es Salaam, Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL, Harbinder Singh Sethi alisema kampuni yake imejizatiti katika kuhakikisha inatekeleza mipango yake ya kusaidia miradi ambayo itaondoa umaskini na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana nchini Tanzania.
Harbinder alisema mpango huo pia unalenga kusaidia shule, makanisa, misikiti na kampuni nyingine zisizotengeneza faida zinapofanya kazi ili kuwawezesha vijana kuwa mstari wa mbele kuchangia maendeleo ya kiuchumi Tanzania
“Tunaamini kuwa Saccos hii itakayoanzishwa itatoa fursa nzuri ya kujiwekea akiba na kutumika kama chanzo cha mikopo kwa vijana na wanakwaya wengine wa kanisa,” alisema.
Naye Katibu na Mwanasheria Mkuu wa IPTL, Joseph Makandege alisema ili kuwapa sauti vijana na kuwaongezea fursa za kujiimarisha kiuchumi, IPTL kwa kushirikiana na Kampuni ya Pan African Power (PAP) imetenga sehemu ya pato lake kwa ajili ya kusaidia miradi ya maendeleo inayowalenga vijana.
“Sisi kama IPTL na PAP, tumeona kuwa ni jukumu letu kuisaidia jamii inayotuzunguka. Kwa kuanzisha Saccos, ninaimani vijana wataweza kuanzisha mradi madhubuti utakaowaletea mabadiliko chanya ya kiuchumi,” alisema Makandege.
Akizungumza kwa niaba ya wanakwaya na waumini, George Kashushura alizishukuru IPTL na PAP kwa msaada na kubainisha kuwa fedha iliyotolewa itaelekezwa katika malengo mazuri yatakayobadilisha maisha ya vijana.